Friday , 27th Nov , 2015

Mahakama kuu ya Tanzania imeandaa mkakati wa ujenzi wa kituo ndani ya mahakama kwaajili ya utoaji wa taarifa muhimu zinazohusu mienendo ya kesi na utoaji taarifa kwa vyombo vya habari.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Jaji Shaban Lila

Mahakama imefikia maamuzi hayo lengo likiwa ni kusaidia upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu kesi ili kuepusha upotoshaji.

Hayo yameelezwa jana na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Jaji Shaban Lila wakati wa ufungaji wa semina ya mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari za mahakama, ambapo alisema kumekuwa na mkanganyiko mkubwa na upotoshaji katika kuripoti taarifa za mahakamani kutokana na wengi kutojua sheria.

Jaji Lila amesema yapo mapungufu mengi katika sheria zilizopo na kuwa mahakama sio watunga sheria ila watafsiri wa sheria na pia kutoa maoni kwa ofisi ya mwanasheria mkuu.

Amesema kuwa zipo lawama nyingi zinazotolewa na wananchi kuhusu maamuzi ya mahakama hizo.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka baraza la habari Tanzania MCT bw. Allan Lawa akitoa baadhi ya maazimio yaliyowekwa na wanahabari hao kusaidia upatikanaji wa taarifa za Mahakamani.

Akitaja baadhi ya maazimio hayo ni pamoja na kuanzisha mtandao wa waandishi wa habari za mahakamani ili kusaidia kurahisha upatikanaji wa taarifa mbalimbali zihusuzo kesi, Mahakama na baraza la habari Tanzania kuanzisha mafunzo yatakayoshirikisha wahariri wa vyombo vya habari, ikiwemo kushawishi kuanzishwa kwa madawati ya habari za Mahakama.