Sunday , 17th Jan , 2016

RAIS wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amefuta rasmi hati ya umiliki wa mashamba makubwa matano yaliyokuwa na hati za miaka 99 yaliyopo Mkoani Tanga yaliyokuwa yamemilikishwa kwa watu waliokuwa wakilima kilimo cha zao la mkonge.

RAIS wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi William Lukuvi katika ziara yake aliyofanya Mkoani Tanga ambapo aMEsema Rais Magufuli alitoa tamko la kufutwa kwa umiliki wa mashamba hayo mnamo tarehe 19 mwezi 12 2015.

Waziri Lukuvi ameyataja mashamba hayo kuwa ni Kikugwi, Sagulasi Estate, Lewa Estate, Bwembwera, pamoja na Azimio yote yaliyopo katika wilaya ya Muheza Mkoani Tanga.

Waziri Lukuvi alisema sababu zilizopelekea Rais Magufuli kutengua hati za umiliki wa mashamba ni pamoja na wawekezaji wa mashamba hayo kuyatelekeza na kupelekea wananchi wa maeneo hayo na maeneo jirani kukosa maeneo ya kufanyia shughuli za kilimo.

Waziri huyo amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mwantumu Mahiza afanye ukaguzi wa mashamba hayo ili ajue mipaka rasmi na kutambua mali zilizopo ndani ya mashamba hayo pamoja na kupeleka mapendekezo ya kuandaa mpango kazi wa matumizi bora ya mashamba hayo.

Waziri Lukuvi amesema wizara yake itadhibiti wimbi la watu wasiotaka kufanya kazi kihalali na badala yake kuwalangua wanunuzi wa viwanja na kuahidi kuwa ifikapo mwezi wa 7 atapunguza kodi ya ardhi ili kila mwananchi aweze kuhimili ujenzi wa nyumba na umiliki wa ardhi kihalali.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mwantumu Mahiza ameahidi kuyafanyia kazi maagizo aliyopewa na Waziri Lukuvi ili kuhakikisha wananchi wanafaidika na ardhi yao pamoja na kupunguza wimbi la migogoro ya ardhi inayojitokeza siku hadi siku.