Monday , 5th Jan , 2015

Jeshi la kujenga taifa JKT, limesema pamoja na ufinyu wa bajeti lakini litaendelea kutatua changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa kikwazo kikubwa kwa vikosi vyake ili kulipa uwezo na nguvu zaidi jeshi hilo.

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Raphael Muhuga

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Raphael Muhuga,ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya awali ya kijeshi ya operesheni miaka 50 ya muungano kundi la pili kwa vijana 627 wilayani Butiama Mkoani Mara, ambapo amesema miongoni changamoto hizo pamoja na ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya vikosi, ununuzi wa zana za kutolea mafunzo pamoja na ulipaji wa madeni ya wazabuni mbalimbali.

Hata hivyo mkuu huyo wa JKT nchini, ameonesha kushangazwa na watu wanaobeza mafunzo hayo ya Jeshi na kusema tangu serikali ikubali kurejesha mafunzo hayo imesaidia kurejesha uzalendo na maadili kwa vijana baada taifa kushuhudia migomo isiyokwisha huku maadili na uzalendo ukipotea.

kwa upande wake mkuu wa kikosi hicho cha 822 KJ Rwamkoma Meja David John Msakulo, amesema kuwa vijana hao kutoka mikoa mbalimbali nchini wamehitimu mafunzo hayo ya awali ya kijeshi ambayo pia yamewajengea umoja na mshikamano mkubwa, huku mmoja wa wasoma risala AKD 8963 SG Leah Evaristi akitaka serikali kufikiria kuongeza muda wa mafunzo kwa vijana wanaojiunga kwa mujibu wa sheria.