Thursday , 30th Jun , 2016

Waziri Mkuu wa Kassim Majaliwa amesema kampeni ya kuhamasisha wadau kuchangia madawati imezaa matunda na kufanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la madawati katika shule za msingi na sekondari.

Akihitimisha mkutano wa tatu wa bunge la 11, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani na kuhamasisha uchangiaji kutoka kwa wadau mbalimbali, jumla ya madawati 552,630 yamepatikana hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu.

Amesema madawati hayo yaliyopatikana yamefanya jumla ya madawati yaliyopo hadi sasa katika shule za msingi na sekondari kufikia 2,672,397 sawa na asilimia 77 ya mahitaji ya madawati yaliyopo.

Amesema upungufu uliopo hadi sasa ni madawati 792,949 sawa na asilimia 23, na kuagiza wakuu wa mikoa na wilaya kushughulikia upungufu huo mara moja kama ambavyo Rais Magufuli aliagiza.

Amesema kwa upande wa shule za sekondari, hadi sasa kuna jumla ya madawati 1,397,138 sawa na asilimia 93 ya mahitaji na kuna upungufu wa madawati 112,885 sawa na asilimia 7%.

Aidha, akizungumzia manufaa ya utekelezwaji wa sera ya ELIMU BURE, Majaliwa amesema kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya wanafunzi ambao wameandikishwa kwa mwaka huu ambapo wanafunzi wa shule za awali walioandikishwa mwaka huu ni 971,717 sawa na ongezeko la asilimia 10.74 ikilinganishwa mwaka 2015.

Kwa upande wa walioandikishwa darasa la kwanza, kwa mwaka huu wameandikishwa wanafunzi zaidi ya milioni 1.8 sawa na ongezeko ya asilimia 36 ikilinganishwa na wanafunzi 1,387,499.