Wakati vikao vya bunge la bajeti ya 2015/ 2016 vikiendelea Mbunge wa Mwibara Mh. Kangi Lugola leo amelipa bunge hilo onesho la bidhaa za nje kabla ya lile la sabasaba linayotarajiwa kuanza mapema mwishoni mwa mwezi huu kwa kuwaonesha bidhaa rahisi kuzalisha ambazo Tanzania imeshindwa kuzitengeneza.
Mh. Lugola amefanya onesho hilo leo katika Bunge la Jamhuri ya Tanzania mjini Dodoma wakati akichangia hoja kwenye majadiliano ya bajeti ya serikali na hali ya uchumi wa taifa, huku akionesha bidhaa kama vijiti vya meno na viberiti, pamba za masikioni vinavyoagizwa kutoka nje ya Tanzania na kusikitishwa na kufa kwa viwanda nchini
Mh Lugola amesema hiyo ni sababu kubwa ya kuporomoka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania na kuitaka serikali kujenga viwanda ili kuzalisha bidhaa hizo kwa ajili ya kuimarisha uchumi na shilingi ya Tanzania
Naye mbunge wa Jimbo la Bahi, Dodoma Nchini Tanzania Mhe. Omary Ahmed Badwel amesema mkoa wa Dodoma unakabiliwa na baa la njaa, ambapo wananchi katika Wilaya ya Bahi kwa sasa wanalala njaa na wengine wanakula vyakula vya ajabu visivyofaa kuliwa na binadamu.
Akichangia Majadiliamo ya Bajeti na Hali ya Uchumi wa Taifa, leo Bungeni, Mhe. Badwel amesema licha ya Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulika na maafa kutoa tani 300 za msaada wa chakula kwa wilaya hiyo, hali bado ni mbaya kupita kiasi
Nao baadhi wa wabunge wakichangia bajeti hiyo wamesema wakulima nchini wamekuwa wakiidai serikali fedha nyingi kutokana na kusuasua kwa mikakati ya kutengwa fedha za Halmashauri pamoja na watendaji wabovu

