Monday , 12th Feb , 2018

Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Antiphas Lissu (CHADEMA) amedai kuwa  jambo moja alilonalo ni kutokukata tamaa na Watanzania.

Lissu ameitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe aliyeko nchini Ubelgiji kwenye safari ya kikazi.

Lissu amesema kwamba anafahamu  kwamba wananchi wapo mbele kimawazo kwa kuwa wanajua wanataka nini na viongozi wamekuwa wakiwa nyuma.

Wananchi wanajua wanataka nini, sisi Viongozi ndio tupo nyuma na Wananchi wapo mbele kimawazo. Jambo moja lipo wazi sana kwangu nalo ni kuwa sikati tamaa na Watanzania,". Lissu

Aidha Zitto amesema kwamba katika mambo waliyozungumza na Lissu huko ni pamoja na suala la uchunguzi wa shambulio lake lililotokea Septemba 7, 2017 huko mkoani Dodoma na kwamba kiongozi huyo amewaomba watanzania kupitia Zitto  waendelee kupaza sauti ili uchunguzi ufanyike na kuwakamata wahusika waliomshambulia. 

"Iwapo watu hawa hawatachukuliwa hatua wataendelea kuumiza watu wengine. Jeshi la Polisi linapaswa kueleza umma limekwama wapi kwenye uchunguzi wa tukio hili baya kabisa kuwahi kutokea katika nchi yetu, la mbunge kushambuliwa kwa risasi katika eneo la Bunge, akihudhuria vikao vya bunge" Zitto Kabwe 

Mbunge Tundu Lissu alishambuliwa na watu wasiojulikana tangu Septemba 7,2017 akiwa mkoani Dodoma, na kisha kupelekwa nchini Nairobi kwa matibabu na baada ya miezi 3 alipelekwa nchini Ubelgiji kwa hatua nyingine ya matibabu