Mbunge wa Arusha mjini (CHADEMA), Godbless Lema (kushoto) na Mbunge wa Kigoma mjini kupitia ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.
Kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter, Lema ameandika, "Nimepigiwa simu na Polisi kwamba natakiwa kuripoti kituo kikuu cha Polisi Arusha leo bila kukosa,sijaelezwa sababu lakini wito unaonekana kuwa wa lazima sana,lakini nafikiri kupigania haki ndio linaweza kuwa kosa langu kubwa. Msiogope".
Mara baada ya kuweka ujumbe huo, Mbunge wa Kigoma mjini kupitia ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amemjibu kwa kuandika, "Wewe kama Waziri Kivuli Mambo ya Ndani umetimiza wajibu wako kupinga utekaji. Watanzania wanajua na Dunia inajua. Wajibu wa Polisi ni kulinda raia na sio kutisha raia. Wajibu wa Mbunge ni kuisimamia serikali likiwemo jeshi la Polisi. Tutashinda".
Jana katika mkutano wake na wanahabari, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro alionesha kuchukizwa na maneno yaliyokuwa yakiandikwa na baadhi ya wanasiasa nchini ambao walikuwa wakikosoa moja ya taarifa yake kuhusiana na kubaini gari lililokuwa limemteka mfanyabiashara Mohammed Dewji kupitia mitandao ya kijamii.
Miongoni mwa wanasiasa ambao walikuwa msitari wa mbele kukosoa hatua hiyo ya IGP Simon Sirro ni Zitto Kabwe na Gobless Lema ambapo kamanda Sirro amesema hajui nia na malengo ya wanasiasa hao.



