Monday , 2nd May , 2016

Chama wa Mawakala wa Forodha nchini Tanzania TAFFA kimesema tishio linalotokana na kupungua kwa mizigo inayoingia na kutoka kupitia bandari mbali mbali nchini hivi sasa lipo dhahiri na sio kificho tena.

Rais wa TAFFA Bw. Stephen Ngatunga

Kutokana na hali hiyo, Chama hicho kimesema kuna haja ya serikali kutodharau tishio hilo na badala yake ichukue hatua za haraka kutokana na madhara ya kiuchumi yanayoweza kuletwa kutokana na kupungua kwa mizigo inayopitia katika bandari zetu.

Rais wa TAFFA Bw. Steven Ngatunga amesema hayo leo katika mahojiano na EATV na kutaja sababu za kupungua kwa mizigo hiyo kuwa ni kutokana na matumizi ya sheria alizodai kuwa sio rafiki kwa ustawi wa biashara na zinazokimbiza wateja hasa wale wanaotoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia, Rwanda, Burundi na Malawi.

"Sisi kama wadau hali hii tulishaiona takribani miaka mitatu iliyopita na tukatoa angalizo kwa mamlaka zinazohusika kuchukua hatua kukabiliana na hali hiyo....lakini badala yake, serikali wakaja na sharia ya ushuru wa VAT kwa mizigo inayokwenda nje ya nchi na hivyo kuwakimbiza wateja," amesema Bw. Ngatunga.

Kwa mujibu wa Bw. Ngatunga, wafanyabiashara kutoka nchi za DRC, Zambia na Malawi hivi sasa wameanza kutumia bandari za Beira nchini Mozambique, Welvis Bay nchini Angola, Cape Town Afrika Kusini na nyinginezo kutokana na mazingira rafiki ya kibiashara yaliyopo katika nchi hizo.

"Kuna meli kumi na sita zilizokuwa zimebeba shehena ya mbolea kwenda DRC, Zambia na Malawi lakini zimelazimika kwenda bandari ya Beira nchini Mozambique kwa sababu ya kukwepa gharama kubwa zinazotoana na matumizi ya sharia ya VAT kwa mizigo inayokwenda nje ya nchi inayojulikana kitaalamu kama Transit Cargo," amefafanua Rais huyo wa TAFFA.

Bw. Ngatunga amefafanua kuwa ushahidi unaonekana hasa katika maeneo ya mipakani na kwamba kupungua kwa mizigo kumeathiri takribani ajira elfu kumi zinazotokana na mnyororo mzima wa usafirishaji mizigo kati ya bandari ya Dar es Salaam na maeneo ya mipakani na kutaja biashara zilizoathirika kuwa ni wauzaji wa mafuta ya magari, wauza chakula maarufu kama Mama Ntilie, wamiliki wa nyumba za kulala wageni kutokana na kupungua kwa wageni wanaolala katika nyumba hizo.