Monday , 13th Oct , 2014

Watu 11 wamethibitishwa kufa maji hadi leo na wengine 10 kujeruhiwa katika ajali ya kuzama mitumbwi miwili waliyokuwa wakisafiria katika ZiwaTanganyika, mkoani Kigoma nchini Tanzania wakati wakitoka kwenye sherehe ya harusi.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma Bw. Jaffary Mohammed amesema jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo lakini sababu za awali inaelezwa kuwa ni kutokana na hali mbaya ya hewa ziwani na kubainisha kuwa hadi sasa haijajulikana ni watu wangapi walikuwemo kwenye mitumbwi hiyo.

Kwa upande wao baadhi ya majeruhi wameelezea kuhusiana na tukio hilo na kusema kuwa idadi ya abiria katika boti hiyo ilizidi kiasi na kwamba kwa dhoruba iliyotokea ndio ikapelekea kuzama kwa mitumbwi hiyo.

Aidha katika hatua nyingine, Tanzania inaongoza barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi kwa kubainika wanawake 66 kati ya laki moja kwa kila mwaka kuwa na saratani hiyo.

Akiongea leo jijini Dar es Salaam, daktari kutoka taasisi ya saratani ya Ocean Road, Dkt. Deonista Kombe amesema katika saratani ya shingo ya kizazi, Tanzania inaongoza kwa kuwa na wagonjwa zaidi ya elfu 40 kila mwaka, huku wanaofika kutibiwa katika taasisi hiyo ni chini ya wagonjwa elfu Tano, ikifuatiwa na saratani ya matiti kwa kuwa na wagonjwa wengi.

Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Sophia Simba amewataka wananchi kujijengea tabia ya kuchangia kuunga mkono jitihada za kuchunguza pamoja na kukabiliana na ueneaji wa saratani ya matiti na shingo ya kizazi.

Wakati huo huo, serikali ya Tanzania imetakiwa kushirikiana na taasisi mbalimbali nchini katika kuboresha sekta ya Elimu kuliko kutegemea misaada ya wahisani na wafadhili kutoka mashirika ya kimtaifa hali inayopelekea kiwango cha elimu kushuka.

Akizungumza jijini Arusha katika uzinduzi wa mradi wa umeme katika kituo cha watoto, Mbunge wa Arumeru Mashariki Mh. Joshua Nassari amesema suala la elimu sio kazi ya kuachia wahisani au mashirika ya kimataifa peke yake bali serikali inatakiwa kutoa mchango wake mkubwa katika kuboresha Sekta hiyo.

Aidha Mh. Nassari ameongeza kuwa suala la Rushwa nalo linachangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa elimu na kuitaka Taasisi ya Kupambana na Rushwa nchini Tanzania TAKUKURU kujiimarisha katika kesi za rushwa zinazochangia taifa kudidimia kwa uchumi.