Thursday , 24th Mar , 2016

Viwanda vidogo vidogo vimetajwa kuwa ndio njia pekee ya kufikia malengo ya uchumi wa viwanda nchini Tanzania kwani viwanda hivyo vinahitaji kiasi kidogo cha mtaji na kuchukua idadi kubwa ya nguvukazi ambayo baadaye huwa fursa za ajira.

Mkurugenzi Mkuu wa taasisi inayojishughulisha na Utafiti wa Jinsi ya Kupunguza Umaskini ya REPOA, Dkt Donald Mmari.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa ndiyo itakayokuwa mwarobaini wa ukosefu wa soko la mazao ya kilimo kwani viwanda hivyo vitakuwa vikitumia mazao hayo kama malighafi kuu inayotumika katika uzalishaji.

Mkurugenzi Mkuu wa taasisi inayojishughulisha na Utafiti wa Jinsi ya Kupunguza Umaskini ya REPOA, Dkt Donald Mmari, amesema hayo katika mahojiano na EATV ikiwa imesalia takribani majuma mawili kabla ya kongamano hilo litakalofanyika jijini Dar es Salaam.

Dkt Mmari amefafanua kuwa ni kwa sababu hiyo ndiyo maana suala la uendelezaji wa viwanda vidogo vidogoni moja ya ajenda kuu zitakazotawala kongamano la kimataifa la masuala ya utafiti litakalofanyika mapema mwezi ujao.

Ajenda nyingine kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji huyo wa REPOA ni pamoja na kuhakikisha kuwa ajenda ya uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo inakwenda sambamba na mipango iliyopo ya kuongeza tija katika kilimo kwa kukigeuza kuwa cha kibiashara.

Dkt Mmari ameongeza kuwa wataalamu waliofanikisha mageuzi ya viwanda katika nchi za China, Indonesia, Marekani na Finland watashiriki kongamano hilo lililoandaliwa na REPOA, ambapo wakiwa nchini watawafundisha washiriki pamoja na wenzao wa Tanzania juu ya jinsi ya kufikia malengo ya uchumi wa viwanda kwa kutumia tafiti, ujuzi na rasilimali zilizopo.