Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova
Kamishna Kova amewataka wakazi wa Dar es salaam kumsaidia kumaliza salama kulitumikia jeshi la polisi leo, kwa kusherehekea sikukuu ya mwaka mpya kwa amani na utulivu.
Akizungumza na East Africa Radio leo Kamishna wa Jeshi la Polisi kanda Maalumu ya Dar es salaam Suleiman Kova amesema kuwa endapo mwananchi atabainika kufanya fujo basi jeshi la polisi halitasita kumchukulia hatua.
Kamanda Kova ameongeza kuwa Jeshi hilo limejipanga katika kuimarisha usalama katika maeneo yote ya jiji huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo pindi watakapoona sehemu kuna viashiria vyovyote vya Uvunjifu wa amani.
Katika hatua nyingine Kamishna Kova ambaye anamalizia muda wake na kustaafu amesema katika kipindi chake cha ustaafu atajiingiza katika masuala ya kusaidia jamii, kujihusisha na siasa pamoja kuanzisha kampuni ya ulinzia ili kuendelea kuisaidia serikali katika kuimarisha usalama.
Aidha Kamanda Kova ameelezea kati ya matukio ambayo yalimpa wakati mgumu wakati wa uongozi wake ni pamoja na matukio ya ujambazi ambayo kwa kiasi kikubwa aliweza kukabiliana nayo, uvamizi wa vituo vya polisi kikiwemo cha staki shari pamoja na usimamizi wa uchaguzi mkuu ambao ulikuwa na mihemko mingi ya kisiasa.