Monday , 22nd Jul , 2019

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga, ameongoza kikao cha viongozi wa juu wa Wizara ya Kilimo, kwa kukutana na Naibu Waziri mpya wa Kilimo Hussein Bashe na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, ikiwa ni saa chache baada ya Bashe kuapishwa na Rais Magufuli.

Katika Kikao hicho wameafikiana kuanzishwa kwa sheria ya Kilimo itakayowezesha kusajiliwa kwa wakulima wa mazao nchini.

Akizungumza na viongozi hao, jijini Dar es salaam, Waziri Hasunga ametoa taswira ya Wizara hiyo, ni kuanza kusajili wakulima wa mazao yote na kuziagiza bodi husika kutoa vitambulisho kwa ajili ya kuwatambua wakulima.

"Kuna kila sababu ya kuanzishwa haraka sheria ya Kilimo na tayari tupo katika hatua za mwisho, kwa sababu hatuna Sheria ya Kilimo, inayotumika sasa ni Sera ya Kilimo, iliyotungwa mwaka 2013 ambayo pia inahitaji kupitiwa upya" amesema.

Hasunga ameongeza, sheria zinazotumika kwa sasa ni za Bodi za Mazao mbalimbali ambazo pia zinachangamoto zake, huku baadhi ya mazao yakikosa bodi na kupelekea hali ngumu ya kuwatetea wakulima.

Mazao yaliyo katika utaratibu wa bodi ni zao la Pamba, Kahawa, Chai, Korosho, Pareto na Tumbaku.