Tuesday , 4th Aug , 2015

Wananchi mkoani Mtwara wamekuwa na maoni tofauti juu ya ujio wa Rais Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete mkoani humo, ambaye atafanya ziara na kuzindua baadhi ya miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na jengo la Benki Kuu ya Tanzania B.O.T Mtwara.

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti hii leo, baadhi yao wameonekana kuibeza ziara hiyo inayotarajiwa kufanyika Agosti 9 mwaka huu kwa kusema ahadi nyingi ambazo aliahidi hazijatekelezwa, huku wengine wakionekana kuvutiwa na ujio wake.

Akizungumzia ujio huo, mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, ametaja maeneo ambayo Rais atatembelea na kuwataka wananchi kuunga mkono na kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya mashujaa ambako atahutubia katika mkutano wa hadhara.

Dendego amesema kuwa Mh. Rais pia tatembelea Kituo cha kusafirishia gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam lakini pia atatembelea kiwanda cha cement cha Dangote pamoja na miradi mingine ya serikali iliyoanzishwa mkoani humo.