
Hayo yameelezwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusema walimkamata Mhe. Rungwe kwa kosa hilo na wala siyo uchochezi kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakisema kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.
"Ni kweli tulimkamata Hashim Rungwe kwa kosa la kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu kutoka kwa waturuki ambao walikuwa wanahitaji msaada wa kisheria kwa ajili ya ununuzi wa Korosho Milioni za 70 ambazo ni sawa na tani 15, tulimkamata Agosti 28, mwaka huu na wala hajakamatwa kwa kosa jingine tofauti na hilo", amesema Kamanda Mambosasa.
Mambosasa amesema Rungwe akiwa wakili anatuhumiwa kushiriki kufanya udanganyifu kwa mfanyabiashara kutoka Uturuki, Suleiman Ysian (48) ambaye alikuja nchini Tanzania kununua korosho tani 15 kutoka kampuni ya Les Tropiques Group Mining Sprl Limited ambapo mkataba wa ununuzi wa korosho unaonyesha una gharama ya Dola 72,000 za Marekani sawa na milioni 161 ambazo zitalipwa kupitia akaunti ya benki ya wakili Rungwe.
Kamanda Mambosasa amesema inadaiwa mfanyabiashara huyo ameshalipa takriban Shilingi milioni 75 lakini hakuna mzigo ulioupata mpaka sasa zaidi ya kuahidiwa tu.
Kwa upande mwingine, mtuhumiwa huyo ataendelea kuripoti katika kituo cha polisi kila siku mpaka pale kesi yake itakapoanza kusikilizwa katika Mahakama.