
HALMASHAURI zote za Mkoa wa Arusha zimetakiwa kutenga bajeti ya michezo na kuhakikisha bajeti hiyo inatumika katika kuinua michezo na kuendeleza vipaji vya vijana katika maeneo yao.
Rai hiyo imetolewa jana jioni na Katibu wa Hamasa na Siasa wa CCM Shabani Mdoe, wakati akikabidhi vifaa vya michezo kwa timu mbili za Mbuguni fC na Shambalai Burka katika mchezo maalum uliofanyika katika shule ya msingi Mbuguni na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa eneo hilo.
Vifaa hivyo vya michezo vilivyokabidhiwa ikiwa ni msaada wa CCM Mkoa wa Arusha vina thamani ya zaidi ya shilingi laki tisa.
Mdoe amevitaja vifaa hivyo ni seti moja ya jezi ,soksi na mipira miwili kwa kila timu ikiwa ni kutekeleza maombi ya timu hizo waliyoyatoa kwa uongozi wa chama hicho mapema mwaka huu na kuzitaka timu zote mbili kutumia vifaa hivyo, kama chachu ya kuwaendeleza vijana katika soka.
Amesema wao kama wanasiasa wana wajibu wa kusaidia katika michezo kwani ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho na pia ni njia ya kuzalisha ajira kwa vijana kwa kua hivi sasa michezo ni ajira.
Pia ametoa wito kwa wawekezaji wanaomiliki mashamba makubwa na taasisi mbalimbali zilizopo Wilayani Arumeru nazo kujitokeza kusaidia michezo katika Wilaya hiyo.
Naye Katibu wa vijana wa Wilaya Hiyo Msafiri Juma Mayeye akiongea kwa niaba ya Vijana wa Wilaya hiyo, ameshukuru kwa msaada huo na kuwataka vijana sasa kutumia vifaa hivyo kuitangaza Wilaya hiyo katika medani za soka.
Amewataka Makapteni wa timu hizo Ally Shabani wa timu ya Mbuguni na Even Laizer wa timu ya Shambalai Burka ,Waliopokea vifaa kwa niaba ya timu zao kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa na kutumika katika mashindano muhimu mbalimbali ndani ya Wilaya na nje ya Wilaya hiyo.