Tuesday , 18th Nov , 2014

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya Sengerema, Liveta Msangi, amepandishwa kizimbani akidaiwa kuchepusha zaidi ya shilingi milioni 11 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ukarabati wa mahakama ya mwanzo wilayani Sengerema.

Msangi amefikishwa katika mahakama ya mkoa wa Mwanza leo ili kujibu tuhuma hizo na kusomewa mashitaka matatu mbele ya hakimu mkazi Abesiza Kalegeya, na mwendesha mashitaka wa serikali Mwema Meila akisaidiana na Martha Mwadenya.

Mashitaka yanayomkabili hakimu huyo ni kuainisha hati ya malipo ya zaidi ya kiasi hicho kwa mwajiri wake kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya mahakama hiyo, shitaka la pili likiwa matumizi mabaya ya mamlaka yake kinyume na kifungu cha sheria namba 31 cha 2007, shitaka la tatu ni kupokea fedha kutoka kwa mwajiri wake kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya mahakama ya Mwanzo Bupambwa wilayani Sengerema.

Wakati huo huo, asilimia 80 ya madini aina ya Tanzanite yanayozalishwa nchini Tanzania, yanatoroshwa nje ya nchi na wafanyabiashara wasio waaminifu, huku nchi ikiambulia asilimia 20 tu ya madini hayo yanayozalishwa eneo la Mererani mkoani Manyara.

Kamishna wa Madini kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Paul Masanja, amesema hayo wakati wa maonyesho ya kimataifa ya Vito, yanayofanyika jijini Arusha na kukutanisha washiriki zaidi ya 500, huku kampuni 69 zikishiriki maonyesho hayo.

Masanja ametoa mfano wa mwaka 2013 ambapo Tanzania ilipata mapato yanayofikia dola za Marekani milioni 38 kutokana na Tanzanite, wakati Kenya walipokea Tanzanite yenye thamani ya dola milioni 100, huku India ikipata dola milioni 300 za madini hayo.

Amesema kuwa kutokana na hali hiyo, serikali imeamua kujenga jengo la kuuzia madini hayo na litakapokamilika hakuna mfanyabiashara atakayeruhusiwa kuuza madini hayo nje ya jengo hilo kama ilivyo sasa.