Monday , 14th Jul , 2014

Wapiganaji wa kundi la waasi katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC la FDLR limeandika barua kwa nchi za Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC ya kuomba kuweka silaha chini na kutaka amani nchini humo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe.

Akitoa taarifa juu ya kundi hilo kwa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini Tanzania, Waziri wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa Benard Membe amesema baada ya kuijadili barua hiyo nchi za SADC wamekubaliana na maombi hayo kwa masharti makubwa matano yakiwemo ya kuwataka wawe raia wa kawaida na kuondoka katika makambi waliyokuwepo na kukaa katika maeneo ambayo watapangiwa.

Hata hivyo waziri Membe amesema Jumuiya hiyo ya SADC imetoa miezi sita kwa waasi hao kuhakikisha wanatekeleza masharti waliyopewa na ikiwemo kutorudi tena katika vita na wakishindwa kutekeleza jumuiya husika ikiwemo ile ya kimataifa wataamua uamuzi sahihi wa kuchukua juu yao

Katika hatua nyingine waziri Membe ameitangaza rasmi Oktoba 9 ya kila mwaka kuwa ni siku ya Dunia kwenye Kaburi la Baba wa Taifa ambapo kupitia siku hiyo mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini watatembelea kijiji cha Butiama ikiwemo kutembelea kaburi la baba wa taifa kwa lengo la kutoa heshima maalum kwa marehemu Baba wa taifa.