Wednesday , 9th Sep , 2015

Imeelezwa kwamba elimu ya afya kuhusu kipindu pindu inatakiwa kutolewa kwa kasi ili jamii ielewe madhara yatokanayo na ugonjwa huo, ambao unaendela kuliathiri jiji la Dar es salaam.

Rai hiyo imetolewa na Muuguzi Kiongozi wa Kambi ya kipindu pindu iliyopo Mburahati jijini Dar es salaam Bi. Shubira Bachuba, alipokuwa akiongea kwa njia ya simu kwenye kipindi cha Super Mix kinachorushwa na East Africa Radio.

Bi Bachuba amesema idadi ya wagonjwa kambini hapo imekuwa ikiongezeka maradufu, na anashangazwa na kitendo cha jamii kulikalia kimya suala hilo.

Amesema hali iliyopo inadhihirisha dhahiri kuwa jamii hususan ya maeneo ambayo yamekuwa yakitoa wagonjwa wa kipindu wengi waliopo kambini hapo, hayana elimu ya kutosha juu ya ugonjwa huu, hivyo kupelekea jamii hiyo kuathiriwa zaidi.

Akiyataja maeneo hayo Bi. Bachuba amesema wagonjwa wengi walipo kambini hapo wanatokea maeneo ya Manzese, Mburahati, Magomeni, Kigogo na Tandale, ingawa pia kuna wagonjwa wanaotoka Mikocheni, Kawe na Bunju.

Bi. Baachuba ameendelea kwa kusema kwamba mpaka jana saa sita usiku, kulikuwa na wagonjwa 46 lakini mpaka leo asubuhi wameshafikia wagonjwa 56, hivyo kuitaka jamii kuwa makini zaidi.