Wednesday , 16th Mar , 2016

Jamii nyingi masikini zimetajwa kuathirika kwa kiwango kikubwa na magonjwa yasiyopewa kipaumbele

Jamii nyingi masikini zimetajwa kuathirika kwa kiwango kikubwa na magonjwa yasiyopewa kipaumbele kutokana na kukosa elimu yakutosha kuhusiana na magonjwa hayo na kuchangiwa na ongezeko lake kutokana na kukithiri kwa imani potofu.

Hayo yamesemwa na mkurugenzi wa taasisi iliyoundwa kwa lengo la kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na magonjwa yasiyopewa kipaumbele Bw. Erick Akaro ambaye ameeleza kuwa magonjwa mengi hayatambuliki katika jamii.

Akiyataja baadhi ya magonjwa hayo ambayo ni miongoni mwa magonjwa yanayo athiri jamii na kuidhoofisha kuwa ni pamoja na Magonjwa ya matende,ngirimaji(mabusha),minyoo ya tumbo,kichocho, trakoma na usubi.

Takwimu kutoka shirika la Afya duniani zinaeleza kuwa takribani watu bilioni moja duniani kote tayari wameathirika, Zaidi ya watu bilioni mbili wako hatarini kupata maambukizi ya magonjwa hayo.

Wakizungumza baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam kwa kueleza uelewa wao kuhusiana na magonjwa hayo wamesema bado elimu inatakiwa kutolewa na wahusika na wataalam wa afya haswa katika maeneo ya vijijini ambako imani potofu zimejikita zaidi.