Tuesday , 1st Sep , 2015

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Mendeleo (CHADEMA) Dkt. Willibrod Slaa leo ametangaza kuachana na siasa, na kusema kuwa atabaki kuwa raia wa kawaida akiwatumikia Watanzania katika kile anachokiamini.

Dkt, Slaa ameyasema hayo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuwepo kwa uvumi kuwa amejitoa katika chama hicho, na kukanusha taarifa kuwa yeye kuwapo likizo.

Dkt. Slaa amesema sababu ya yeye kujitoa kwenye chama hicho na kuamua kuachana na siasa moja kwa moja ni kutofautiana kwa makubaliano na viongozi wa CHADEMA, kuhusu suala la kumpokea mgombea urais kupitia CHADEMA Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Edward Lowassa ambaye alikuwa CCM.

“Niliamua kuachana na siasa baada ya kuona mambo hayaendi sawa kama nilivyotegemea ndani ya chama changu, tulibishana na viongozi akiwemo Mch. Gwajima tangu saa 3 hadi saa 9 lakini hakukuwa na majibu ya kuridhisha, niliandika barua ya kujiuzulu lakini Prof. Abdalah Safari akaichana, sikukata tamaa nikaandika tena,” alisema Dkt. Slaa.

Dkt. Slaa amendelea kwa kusema kuwa kwa kipindi chote alichokuwa kimya amekuwa akipata vitisho vikali vya kuhatarisha uhai wake, kuliko vile alivyokuwa akivipata wakati alipotangaza orodha ya List of ShamDkt. Slaa pia ameongelea suala la kuhamia CHADEMA Mhe. Edward Lowassa baada ya kukatwa CCM, na kusema kuwa yeye binafsi hakuwa na pingamizi juu ya hilo, lakini alitaka wampate mgombea msafi aliyekuwa na sifa zote.

“Si kwamba nilikuwa sitaki Lowassa agombee urais, nilitaka tupate mgombea mwenye sifa zote, sikuambiwa lolote kama Lowassa ni asset au liability ndani ya chama chetu na ndio maana nilikuwa sielewi, wakati hayo yanaendelea nilikuwa nasimamia uteuzi wa viongozi mbalimbali ndani ya CHADEMA,” alisema Dkt. Slaa.

Dkt. Slaa aliendelea kwa kusema kuwa taarifa zilizozagaa kwa wananchi kuwa yeye kama Katibu Mkuu alikubali tangu mwanzo kumpokea Mhe. Lowassa, hazina ukweli wowote, badala yake alitaka baada ya kuingia kwenye chama hicho ajisafishe tuhuma zake za rushwa kwa kutoa vielelezo.

“Upotoshwaji kwamba Dkt. Slaa alikubali tangu mwanzo si kweli naomba viongozi wangu waseme kweli, swali la Asset sikupata majibu, ndio maana hadi leo viongozi wangu wamepata kigugumizi, kuongelea kwanini nimeondoka,” alisema Dkt. Slaa.

Dkt. Slaa alimaliza kwa kusema kuwa amestaafu siasa na atabaki kuwa mtetezi wa wanyonge, na afadhali apotee kwenye siasa Tanzania na duniani kote, kuliko kuyumbishwa na misimamo yake.