Waziri wa afya na ustawi wa jamii Dk. Seif Rashid pamoja na naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Canada Mh. Marcolm Brown wamezindua jengo la upasuaji katika kituo cha afya Sangabuye wilayani Ilemela lililojengwa kwa msaada wa serikali ya Canada kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni mbili ikiwa ni jitihada za kupunguza vifo vya akinamama vitokanavyo na uzazi, watoto wachanga na watoto chini ya miaka mitano.
Dk. Seif Rashid amesema katika kuhakikisha vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto vinapungua, watoa huduma zaidi ya 600 katika jamii wamepatiwa mafunzo ya kuelimisha jamii umuhimu wa kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya, huku pia watoa huduma za afya ya uzazi na mtoto zaidi ya 2,000 wakijengewa uwezo kwa kupatiwa stadi za kuokoa maisha katika ngazi za vituo vya kutolea huduma za afya.
Kwa upande wake naibu waziri wa mambo ya nje wa Canada Malcolm Brown aliyefuatana na balozi wa Canada hapa nchini, amesema Tanzania ni moja ya nchi za Afrika ambazo zimepewa kipaumbele katika kufadhiliwa na serikali ya Canada katika suala la afya ya mama na mtoto kutokana na mahusiano ya karibu zaidi yaliyopo kati ya Rais Dk. Jakaya Kikwete na waziri mkuu wa Canada Stephen Harper katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto vinavyoweza kuzuilika.
Mradi wa wazazi na mwana unaotekelezwa katika wilaya tano za Nkasi, Sumbawanga vijijini na Kalambo mkoani Rukwa pamoja na wilaya za Ilemela na Sengerema mkoani Mwanza chini ya ufadhili wa shirika la maendeleo la kimataifa la Canada unatekelezwa chini ya ushirikiano wa wizara ya afya, Plan International, Jhpiego na Africare.