Makamu wa rais wa Tanzania Dkt Mohammed Gharib Bilal.
Akizungumza na East Africa Radio Kaimu Katibu Mtendaji wa (MCT) John Mireny, amesema kuwa mkutano huo utafanyika Jijini Dar es Salaam kesho ukiwa na lengo la kuwezesha mazungumzo uwazi na kukuza mahusiano mazuri ya kazi kwa vyombo vya habari na vyombo mbalimbali vya serikali.
Aidha, Mireny amesema kutakuwepo na mada tatu zitakazowasilishwa na kujadiliwa wakati wa mkutano huo na moja ya mada itakuwa jinsi ambavyo vyombo vya sheria vinaweza kukuza uhuru wa kujieleza na juu ya ulinzi kwa waandishi wa habari za uchunguzi na wandishi wa habari za kawaida kwa ujumla.
Wakati huo huo, Tanzania bado inakabiliwa na idadi kubwa ya vifo vya wakina mama wajawazito na watoto wadogo ambapo takwimu zinaonyesha kuwa wastani wajawazito 437 hufariki dunia katika kila vizazi hai laki moja.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Afya Tanzania, Daktari Omar Chillo, amesema hayo leo wakati akizungumzia kongamano la kitaifa la masuala ya afya litakalofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo ametaja moja ya chanzo cha vifo hivyo kuwa ni huduma duni za afya ya uzazi pamoja na maambukizi ya magonjwa hatari kama malaria.
Kwa mujibu wa Daktari Chillo, ni kwa sababu hiyo ndiyo maana wameitisha kongamano hilo ambalo amesema pamoja na mambo mengine, litawakutanisha wadau muhimu wa sekta ya afya ambao watajadili na kutafuta suluhu zinazoikabili sekta ya afya ikiwemo tiba na kinga kwa magonjwa yanayoweza kuepukika.
Aidha, imeelezwa kuwa zaidi ya asilimia 50 ya wanawake ambao ni wagonjwa wa saratani wanaotibiwa katika Taasisi ya saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam, wamebainika kuwa na saratani ya shingo ya kizazi huku wengi wao hawafahamu dalili za ugonjwa.
Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam na daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka taasisi ya saratani ya Ocean Road Dkt. Chakou Hassan wakati alipokuwa akizungumza na East Africa Radio juu ya hali ya ugonjwa huo hapa nchini.
Amesema japokuwa saratani ya shingo ya kizazi hapo awali ilikuwa ikiwapata zaidi wanawake wazee lakini kwa sasa hali imebadilika kutokana na kuwapata wakina mama ambao ambao siku zao za hedhi zimekoma.