Wanafunzi wakiwa Darasani wakimsikiliza mwalimu(Picha na Maktaba)
Kwa mujibu wa Mwalimu mkuu wa shule hiyo Grace Mkoloma, darasa la kwanza lenye wanafunzi 278 lina dawati moja pekee lililopelekwa shuleni hapo na mzazi wa mwanafunzi mmoja ambaye hakutaka mtoto wake akae chini.
Uwepo wa dawati hilo moja unatoa fursa kwa mtoto wa mzazi huyo kuteua rafiki zake wengine wawili kukalia dawati hilo wakati wa masomo hivyo wanafunzi wengine 275 hulazimika kukaa chini.
Mwalimu Mkoloma amebainisha hayo kwenye mkutano wa wazazi na wadau wa elimu shuleni hapo uliofanyika jana ukiwa na lengo la kuelimisha jamii juu ya dhana ya Sera ya Elimu bure pamoja na kujadili changamoto inayoikabili shule hiyo ikiwemo mlundikano wa wanafunzi madarasani pamoja na uhaba wa madawati.
Amesema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 2000 wa kuanzia darasa la awali hadi la saba na wanafunzi wa darasa la kwanza pekee wapo 278 kati yao ni wanafunzi watatu tu ndio wanaokaa katika dawati moja lililotengenezwa na mmoja wa wazazi wa mtoto ambaye alifika shuleni hapo na kukuta mwanae anakaa chini wakati akisoma.
Mkuu huyo wa shule alisema kwa sasa uhitaji wa madawati shuleni hapo ni madawati 463 kwani kwa sasa shule ina madawati 248 ambayo yamegawanywa katika vyumba vya madarasa 11,hivyo kuiomba serikali na jamii kulitazama suala hilo na kulipatia ufumbuzi haraka iwezekanavyo ili kunusuru watoto hao kutofanya vibaya kitaaluma.
Mmoja wa wajumbe wa kikao hicho Mussa Mlele alisema wao kama wazazi wamesikitishwa na hali hiyo hivyo kuwataka wazazi wenzake kuungana pamoja ili kutafuta ufumbuzi wa tatizo la madawati shuleni hapo badala ya kungoja serikali akisema wanaoumia ni watoto wao wazo lililoungwa mkono na wananchi wenzake.