Friday , 16th Oct , 2015

Mwenyekiti wa chama cha National League For Democracy (NLD) na Mgombea ubunge wa jimbo la Masasi, Dkt. Emmanuel Makaidi, amefariki dunia akiwa katika hospitali ya Nyangao, wilaya ya Lindi vijijini mkoani Lindi, kutokana na kuugua shinikizo la damu.

MWENYEKITI Mwenza wa Ukawa na Mwenyekiti wa chama cha NLD, Emmanuel Makaidi

Kwa mujibu wa kaimu mganga mkuu aliyethibitisha kifo chake kutoka katika hospitali hiyo, Dkt. Betram Makota, amesema marehemu alifikishwa hospitalini hapo majira ya saa tano asubuhi na mkewe huku hali yake ikiwa mbaya zaidi ambapo alifariki dunia majira ya saa saba mchana.

Amesema, alianza kuugua siku mbili zilizopita na kupelekwa katika zahanati moja huko wilayani Masasi na kupata matibabu ambayo, lakini alivyoamka jana hali ilibadilika na kuishiwa nguvu ndipo ikaamuliwa akimbizwe hospitalini hapo.

Amesema kwa mujibu wa ndugu zake, maiti inatarajiwa kusafirishwa kesho kwenda jijini Dar es Salaam kwa ajili ya shughuli za mazishi.

Kifo cha Dk. Makaidi kinafanya idadi ya wagombea ubunge waliofariki katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi kufikia watano, wakiwemo Mohammed Mtoi wa CHADEMA, Celina Kombani wa CCM, Estomih Mallah wa ACT-Wazalendo na Dk. Abdallah Kigoda wa CCM.