Monday , 10th Nov , 2014

Chama cha Walimu nchini Tanzania kimekanusha madai ya serikali kuwa imelipa kwa asilimia kubwa madai ya malimbikizo ya waalimu na kubaki malimbikizo ya kiasi cha shilingi bilioni 4 tu na kusema kuwa kauli hiyo ya serikali haina ukweli wowote.

Rais wa Chama cha Walimu nchini Tanzania (CWT) Mwalimu Gratian Mukoba.

Akiongea na East Africa Radio Rais CWT, nchini Bw. Gratian Mukoba amesema wamegundua kuwa kuna walimu ambao wanadai kiasi kikubwa cha fedha wamewekewa kiasi kidogo sana tofauti na serikali ilivyosema.

Bw. Mukoba amesema deni lililobaki ni zaidi ya shilingi bilioni kumi na kuwa walimu wengi wamelipwa isivyotarajiwa na sasa wanampango wa kulikusanya tena deni lao kwa sababu deni bado ni kubwa na serikali imefanya kidogo sana katika kumaliza au kulipunguza deni hilo.

Wakati huo huo, serikali ya Tanzania imesema iko katika mpango wa kuandaa utaratibu wa kuziweka alama dawa ili kuweza kudhibiti wizi wa dawa uliopo kwa sasa kwa baadhi ya watumishi wa afya kujinufaisha na dawa hizo kutoka serikalini.

Akijibu swali kwa Niaba ya Waziri Mkuu leo Bungeni Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaje Mh. Amosi Makalla amekiri kuwepo kwa baadhi ya watumishi wanaotumia mwanya uliopo sasa kuweza kuhujumu upatikanaji wa dawa nchini.

Aidha, Makala ameongeza kuwa serikali kwa kupitia Wizara mbalimbali wameshakutana kwa ajili ya kuweza kutafuta njia za haraka za kuweza kulipa deni la MSD ili kuweza kuanza kusambaza kwa wananchi kama kawaida.