Sunday , 7th Sep , 2014

Benki Kuu ya Tanzania leo imezindua sarafu ya shilingi mia tango, itakayoanza kutumika mwezi ujao na kuchukua nafasi ya malipo pamoja na matumizi yote halali yanayofanywa kwa kutumia noti ya sasa ya shilingi mia tano.

Mkurugenzi wa Huduma za Kifedha za benki hiyo Bw. Emmanuel Boaz ametaja sababu za kutoa sarafu hiyo kuwa ni kutokana na kuchakaa haraka kwa noti ya shilingi mia tano kunakochangiwa na noti hiyo kutumiwa na idadi kubwa ya watu katika matumizi yao ya kila siku.

Bw. Boaz amefafanua kuwa sarafu hiyo itatumika wakati hatua za kuiondoa noti ya shilingi mia tano katika mzunguko ikiendelea taratibu pasipo kuathiri upatikanaji wa fedha kwa ajili ya malipo ya shilingi mia tano.

Awali, Mkurugenzi Msaidizi wa idara ya mahusiano na Protokali ya benki hiyo Bi. Victoria Msina amesema hatua ya mabadiliko ya muundo wa noti ya mia tano kwenda sarafu ni majukumu ya kawaida katika kuhakikisha aina na ubora wa fedha zinazotumika katika malipo na manunuzi zinakidhi viwango.