Saturday , 27th Jun , 2015

Mkoa wa Arusha umepiga marufuku tabia iliyozuka ya baadhi ya vijana kuwauzia nafasi watu wanaojiandikisha katika daftari la wapiga kura, kwa mtindo uliobatizwa jina la “KUUZA PLOT”

Daudi Ntibenda

Mkoa wa Arusha umepiga marufuku tabia iliyozuka ya baadhi ya vijana kuwauzia nafasi watu wanaojiandikisha katika daftari la wapiga kura, kwa mtindo uliobatizwa jina la “KUUZA PLOT”

Mtindo huo umezuka na kuwa sehemu ya kujipatia kipato kwa baadhi ya vijana, ambapo wamekuwa wakiwahi foleni katika vituo vya kujiandikishia, na baadaye nafasi hizo kuwauzia watu waliochelewa ambao hawataki kukaa muda mrefu kwenye foleni hizo.

Akizungumza na wananchi wa kata ya Sekei waliojitokeza katika zoezi la uandikishaji kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Daudi Ntibenda amepiga marufuku tabia hiyo baada ya kubainika kwa vijana wanaokesha katika vituo vya uandikishaji wakiwahi nafasi kwaajili ya kuwauzia watu wengine.

Katika zoezi hilo la awamu ya pili linalozijumuisha kata sita za Jiji la Arusha,baadhi ya wananchi waliojitokeza kujiandikisha kwa upande wao wamelalamikia kasi ndogo ya uandikishaji, huku Mkurugenzi wa Jiji hilo Juma Iddi akibainisha kwamba jumla ya mashine 130 zimekwishapelekwa katika vituo vilivyotengwa kwaajili ya kukamilisha zoezi hilo kwa muda uliopangwa.

Taarifa kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Arusha lenye kata 25 na mitaa 154, hadi kufikia sasa jumla ya watu 85,234 wamekwishaandikishwa ambapo kwa mujibu wa ratiba zoezi la uandikishaji mkoani hapa linatajiwa kuhitimishwa july 19 mwaka huu.