Saturday , 15th Sep , 2018

Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Paul Makonda, pia mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani humo, amewahakikishia wakazi wa Ukonga kesho siku ya Jumapili kuondoa hofu ya kutojitokeza kupiga kura kwa ahadi ya kuwepo amani na utulivu katika zoezi zima.

Mh. Paul Makonda

Ikiwa wagombea Asia Msangi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), na Mwita Waitara kupitia CCM ndio itakuwa hatima yao kesho, wananchi wamehimizwa kuwa huru kupata haki yao kumchagua wampendaye.

Akisisitiza Makonda, ''Tumejipanga kuhakikisha kwamba hakuna tishio lolote lile litakalofanywa na kumfanya mwananchi asite kwenda kupiga kura, asite kwenda kumchagua mgombea anayemtaka, kwa hiyo naomba niwahakikishie kamati yetu ya usalama nikiwa mwenyekiti wake ya kwamba, hari ni shwari kuna utulivu wa hali ya juu na nyie wenyewe ni mashahidi hata kampeni zimeendeshwa  kwa ustaarabu kwa asilimia kubwa ndani ya mkoa wetuwa Dar es Salaam''

Pia amesema, kuhakikisha usalama zaidi, uchaguzi utafuata sheria ya tume ya uchaguzi ya kupiga kura na kumlazimu mtu kuondoka eneo la tukio ili kufisha uchochoezi na vurugu zisabababishwazo na makundi ya watu ''tumejifunza kipindi cha nyuma, hatutaki makosa hayo yaweze kujirudia tena ndani ya mkoa wa Dar es Salaam''

Mwisho Makonda amewasihi wananchi wote, wanasiasa na vyama kuyapokea matokeo kwa pande zote mbili kushinda ama kushindwa, na sio kufanya fujo kupelekea kuuchafua mji wa Dar es Salaam ambao ni kitovu cha biashara hapa nchini, pia kivutio kikubwa kwa wageni.

''Asiyekubali kushindwa si mshindani, matokeo tutakayoyapata kupitia viongozi waliochaguliwa na tume ya uchaguzi tuyapokee na twende tuyashangilie kwa amani tusifanye fujo'' ameonya Makonda.

Uchaguzi huu mdogo unafanyika sehemu mbili, majimbo ya Monduli  na Ukonga ikiwa ni kutokana  na wabunge wake kwa tiketi ya CHADEMA, Julius Kalanga kwa upande wa Monduli na Mwita Waitara kwa upande wa Ukonga kujiuzulu huku wakiwania tena nafasi hiyo ya ubunge kupitia CCM.