Tuesday , 25th Aug , 2015

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini imesema watu 7 wamekufa na ugonjwa wa kipindupindu huku wagonjwa 230 wakilazwa katika kambi mbali mbali katika mikoa ya Dar es salaam na Morogoro.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijin Dar es salaam Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid amesema kuwa Kati ya wagonjwa hao 194 ni kutoka Dar es salaam na 36 ni kutoka Mkoa wa Morogoro.

Dkt. Seif amesema ili kupambana na ugonjwa huo serikali imewaagiza maafisa Afya wa Kata zote nchini kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa Afya katika kaya, Shule na Vyuo vyote nchini ili kuhakikisha mazingira yapo safi muda wote huku kanuni zote za Afya zikifuatwa.

Aidha Dkt. Seif ameongeza kuwa watashirikiana na Idara ya Maji ili kutibu vyanzo vyote vya maji pamoja na kuwataka wananchi wote kuweka mazingira ya vyoo hasa vya shimo katika hali safi, huku akiwataka mama lishe kuzingatia usafi.