Ijumaa , 2nd Feb , 2018

Kuelekea mchezo wa ligi kuu raundi ya 16 kesho kati ya wenyeji Lipuli FC dhidi ya Yanga SC Afisa Habari wa wanajangwani Dismas Ten amedai watapambana kadri ya uwezo wao kupata matokeo yaliyokuwa mazuri ili waweze kuutetea ubingwa wao wasije kuupoteza

Kikosi cha Yanga kikiwa kinajifua

Dismas ameeleza hayo wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari mkoani Iringa ambako ndipo utachezwa mchezo huo majira ya saa 10:00 alasiri katika uwanja wa Samora. 

"Mara nyingine kucheza ugenini unapata shida kidogo lakini ni utaratibu wa mpira duniani kote, ligi inachezwa nyumbani na ugenini kwa hiyo sio jambo geni kwetu. Tumejiandaa kwa sababu tunafahamu huu mchezo upo kwa mujibu wa ratiba", alisema Dismas.

Pamoja na hayo, Dismas aliendelea kwa kusema "tunajua Lipuli FC wapo nyumbani na wanamashabiki wengi, tunafahamu ubora wao kwa namna walivyokuwa wanapata matokeo katika michuano ya ligi kuu kwenye michezo iliyopita. Tupo tayari kwa mapambano na lengo tu ni moja tu ambalo ni kutafuta matokeo ili tuweze kuwa nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi na kuutetea ubingwa wetu".

Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara timu ya Yanga imeshika nafasi ya tatu kwa alama 28 huku mpinzani wake Lipuli FC akiwa nafasi ya 7 kwa alama 16 ambapo kilele kinashikiliwa na Simba SC kwa alama 35 akifuatiwa na Azam FC kwa alama 30.