
Rais John Magufuli leo amelihutubia bunge kwa mara ya kwanza na kulizindua rasmi licha ya wabunge wa vyama vya UKAWA kutolewa bungeni kwa agizo la Spika baada ya kufanya fujo bungeni.
Katika hotuba yake Magufuli amesisitiza agizo lake la kufuta safari za nje ambazo kwa mwaka 2013/14 amesema kuwa ziliigharimu serikali zaidi ya bilioni 300.
Rais huyo wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amesema atahakikisha kero mbalimbali zinazowakabili wananchi zinashughulikiwa kwa haraka ikiwa ni pamoja na kuimarisha muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Akilihutubia Bunge la 11 kwa mara ya Kwanza Dkt. Magufuli amesema anatambua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi hivyo ni wajibu wa wabunge kushikamana pamoja kuzishughulikia.
Dkt. Magufuli amesema katika awamu hii amepanga kuimarisha mihimili ya dola ikiwa ni pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi.
Dkt John Pombe Magufuli, amewataka watendaji wa serikali kuacha urasimu unaokwamisha uwekezaji na ukuaji wa uchumi nchini na kwamba kamwe hatasita kuwachukulia hatua watumishi wote wazembe wasioendana na falsafa yake ya “Hapa Kazi Tu”.
Magufuli amesema Tanzania ina kila aina ya fursa zinazoweza kuleta mabadiliko chanya ya kiuchumi lakini urasimu na uzembe katika baadhi ya taasisi za umma umesababisha hata wawekezaji wakimbilie nchi za jirani.
Rais Magufuli amewataka watumishi wa serikali kuhakikisha ahadi yake ya ujenzi wa viwanda inatekelezeka kwa kuhakikisha kuwa mipango inaelekezwa katika kujenga viwanda vya uongezaji thamani bidhaa za mashambani na mifugo, ili Tanzania iwe kitovu cha viwanda huku bidhaa zake zikipata masoko mazuri ndani na nje ya nchi.
Magufuli ameahidi kupambana na wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya pamoja na wala rushwa na mafisadi na amewaomba Watanzania wamuunge mkono katika vita hivyo na kumuombea kwa Mungu.
Rais Magufuli amesema tatizo la dawa za kulevya limekuwa likiathiri vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa, jambo ambalo halipaswi kuachiwa.
Kuhusu tatizo la rushwa Dk. Magufuli amesema anaichukia rushwa na kama alivyoahidi katika kampeni zake kuwa atapambana nayo, atapambana na wala rushwa na mafisadi na hatakuwa na huruma kuwashughulikia..
Aidha,Dkt.Magufuli amesema katika mchakato wa Kupatikana kwa katiba mpya amesema anatambua kazi iliyofanywa na wananchi katika kutoa maoni yao pamoja na kazi ya bunge na atarekebisha sheria ili kuhakikisha katiba mpya inapatikana
Aidha, Dkt. Magufuli amesema katika mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya amesema anatambua kazi iliyofanywa na wananchi katika kutoa maoni yao pamoja na kazi ya bunge maalum la katiba hivyo serikali yake itarekebisha sheria ili kuhakikisha katiba mpya inapatikana.
