Ijumaa , 11th Nov , 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewahakikishia Wasanii kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Mhe. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuunga mkono wasanii wote, kwa kuhakikisha sekta za Utamaduni, Sanaa na michezo zinaendelea kuwanufaisha vijana wengi

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza katika uzinduzi wa Tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni linalofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Novemba 11, 2022 Bagamoyo mkoani Pwani.

Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango ametoa kauli hiyo Novemba 11, 2022 wakati akifungua Tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni linalofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa).

“Sanaa ndiyo roho ya taifa lolote, hatuna budi kuhakikisha tuna Sanaa yenye asili na maadili yanayotuwakilisha sisi Watanzania, nawasihi Watanzania wenzangu na hasa wasanii wetu wa kizazi kipya kuepuka tabia ya kuiga kila tamaduni bila kuchuja wala kuzingatia maadili yetu” amesema Mhe. Dkt. Mpango.

Amesisitiza kuwa, Pale inapolazimika kuiga Sanaa na tamaduni za mataifa mengine, basi wahakikishe wanaiga Sanaa zinazoendana na maadili ya tamaduni zetu, bila kupoteza asili, heshima na utambulisho wa Tanzania.

Makamu wa Rais ametoa rai kwa wasanii wa muziki na filamu kuhakikisha wanazingatia maadili na miongozo ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Bodi ya Filamu Tanzania kwa kutengeneza maudhui yanayokubalika solo la ndani na nje.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewataka wasanii kutengeneza taswira nzuri katika jamii, ambayo haitawafanya walezi na wazazi kuwa wagumu kuruhusu vijana wao kujihusisha na Sanaa kupitia muziki na filamu.

Aidha, Makamu wa Rais Dkt. Mpango ametoa maagizo nane kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ya kuendelea kusimamia sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo kikamilifu ili ziendelee kuwa na mchango thabiti katika uchumi wa taifa, kuendelea kusimamia shughuli za michezo na Sanaa vema kuanzia shuleni kwa sababu sasa zinatambuliwa kama taaluma kamili na ajira.

Vilevile kwa viongozi katika mamlaka zote za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa waendelee kushirikiana na Wizara yenye dhamana katika kuendeleza shughuli za Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na kuyalinda maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli hizo.