Ijumaa , 15th Dec , 2017

Timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) itamkosa mchezaji wake mahiri mlinzi wa kushoto Mwinyi Haji Mngwali kwenye mchezo wa nusu fainali ya CECAFA dhidi ya Mabingwa watetezi Uganda jioni ya leo.

Mchezo huo ambao utaamua nani aende fainali kucheza na wenyeji Kenya ambao tayari wameshatangulia utapigwa kwenye uwanja wa Moi mjini Kisumu nchini Kenya.

Mwinyi anatumikia adhabu ya kadi mbili za njano alizopata kwenye mechi mbili mfululizo zilizopita ambazo ni dhidi ya Kenya ambapo timu hizo zilitoka sare ya 0-0 na ule dhidi ya Libya ambapo Zanzibar ilipoteza kwa bao 1-0.

Kocha wa kikosi hicho Hemed Morocco amethibitisha kuwa mwinyi atakosekana katika mchezo huo na nafasi yake  itazibwa na mlinzi Adeyum Ahmed Seif  ambaye pia ana uwezo mkubwa.

Katika nusu fainali ya kwanza iliyopigwa jana jioni wenyeji wa michuano hiyo Kenya walitinga fainali kwa kuifunga timu ya taifa ya Sudan.