Alhamisi , 16th Jun , 2022

Uongozi wa klabu ya Yanga umethibitisha kuwaandikia barua waandaji wa shindano la Nani Zaidi, kujiondoa rasmi kwenye shindano hilo linalohusisha mashabiki wa vilabu vya Simba na Yanga kuchangia vilabu vyao.

Msemaji wa Yanga Haji Manara

Msemaji wa Yanga Haji Manara amethibitisha kwa mabingwa hao wapya wa ligi kuu Tanzania Bara kwa msimu 2021/22 kuwaandikia kampuni ya Azam PayTv ambao ni waandaji wa shindano hilo lililozinduliwa mnamo Juni 2,2022 jijini Dar es Salaam.

“Ni kweli tumeandika barua ya kujitoa kwenye shindano la Nani Zaidi,lakini klabu itatoa taarifa rasmi kwa nini tumeandika barua ya kujiondoa kwa sababu haya mambo yanahitaji sheria kuyaelezea“’amesema Manara

Katika hatua nyingine,Manara ameelezea kuhusu utaratibu wa kukabidhiwa kombe lao la ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara kwa msimu huu ambapo watakabidhiwa kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City utakaofanyika kwenye dimba la Sokoine jijini Mbeya mnamo siku ya Juni 25,2022

Yanga inaingia kambini kesho kujiwinda na mchezo wa ligi kuu Tanzania bara dhidi ya Polisi Tanzania ambapo klabu hiyo utatumia mchezo huo kuwaaga mashabiki wao kwani utakuwa mchezo wa mwisho kucheza kwa msimu huu kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa,Jijini Dar es Salaam.