Jumatano , 25th Mei , 2022

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Yanga Hassan Bumbuli amejinasibu kuwa rekodi zinawabeba dhidi ya Simba katika michezo waliocheza Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.

Yanga watacheza dhidi ya Simba kwa mara ya 4 msimu huu

Miamba hii ya soka nchini itakutana Jumamosi hii Mei 28 katika uwanja wa CCM Kirumba kwenye mchezo wa hatua ya nusu fainali ya michuano ya Azam Sports Federation Cup. Kuelekea mchezo huu Bumbuli amesea Jiji la Mwanza na uwanja wa Kirumba ni nyumbani kwa Yanga na anaamini hii inatosha kuwapa matokeo katika mchezo huo utakaocheza majira ya Saa 9:30 Alasiri.

 

''Uwanja wa CCM Kirumba ni uwanja wa nyumbani wa Yanga, na tukizungumzia Mwanza ni sehemu ya nyumbani ya Yanga. Katika mechi 4 maarufu ambazo zinakumbukwa hapa Mwanza, ni ile ya mwaka 1975. Ile ndo mechi inayoshikiria rekodi kubwa zaidi na inakumbukwa zaidi ya magoli 2-1, ambayo tulishinda. Katika miaka 20 iliyopita Simba ilipata ushindi mechi moja, lakini zilizofata tuliwapiga 3 taliwapiga 1-0.'' Amesema Bumbuli.

Kwa upande mwingine Bumbuli amethibitishwa kuwa kikosi hicho kitarejea jijini Mwanza siku ya Ijumaa Mei 27, kikitokea mkoani Shinyanga ambako kimeweka kambi ya mazoezi kujiandaa na mchezo huo wa nusu fainali dhidi ya watani zao. Na ameweka wazi kuwa hakuna mchezaji hata mmoja mwenye majeruhi wachezaji wote wapo vizuri kuelekea mchezo huo.