Jumatano , 22nd Mar , 2023

Kikosi cha klabu ya Yanga kinataraji kuondoka nchini Jumanne ya Machi 30 kuelekea nchini DR Congo kwa ajili ya mchezo wa kuhitimisha hatua ya makundi michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya TP Mazembe utakaochezwa Jumapili Aprili 2, 2023.

Afisa Habari wa klabu ya Yanga, Ali Kamwe amesema wanaendelea na maandalizi ya safari hiyo lakini amesisitiza licha ya kwamba wameshatinga robo fainali ya michuano hiyo lakini bado wanauhitaji ushindi dhidi ya TP Mazembe mabingwa wa zamani wa kombe hilo.

"Tunajivunia kuwa na mashabiki bora kwenye Klabu na hili tumelidhibitisha kwenye michezo yetu mitatu ya Kimataifa tukiwa nyumbani na sasa Uongozi wa Klabu umeamua lazima usafiri na mashabiki wake kwenda nao Congo kwenye mchezo wetu wa mwisho kwenye hatua ya makundi"amesema Kamwe

Kwa upande mwingine:Ali Kamwe ametangaza kuwa kutakuwa na uratibu mzuri wa Usafiri kwa mashabiki, wanachama na wapenzi wa klabu hiyo kwa ajili ya kwenda nchini DR Congo kuutazama mchezo huo.

Vile vile Yanga SC imethibitsha kuwa itawakosa nyota wake watatu kwenye mchezo huo, Mlinda mlango Djigui Diarra, kiungo Khalid Aucho na beki Djuma Shabani ambao wanakosekana kwasababu za kikanuni baada ya kuoneshwa kadi za njano mfululizo.

Yanga SC ndiye kinara wa kundi D ikiwa na alama 10 sawa na US Monastir ya Tunisia ambao wanatofautiana kwa magoli ya kufunga na kufungwa, TP Mazember watatu akiwa na alama 3 huku AS Real Bamako ya Mali ikishika mkia ikiwa na alama 1.