Jumanne , 16th Aug , 2022

Klabu ya Manchester United inafikiria kumruhusu Cristiano Ronaldo kuondoka Old Trafford kabla ya dirisha la usajili la sasa kufungwa kufuatia kuwepo kwa wasiwasi kwamba hali ya mshambuliaji huyo inaathiri ari ya kambi.

Cristiano Ronaldo mshambuliaji wa Manchester United

Kwa muda mrefu msimamo wa kocha Erik ten Hag umekuwa kwamba Ronaldo hauzwi na ni sehemu ya mipango yake katika kikosi hicho, lakini vipigo vya mfululizo vya ligi kuu dhidi ya Brighton na Brentford vimetikisa vibaya United, na sehemu kubwa ya kushindwa huko imewekwa kwa Ronaldo.

Nyota huyo wa kireno mwenye umri wa miaka 37, amekua akiishi kana kwamba hayupo katika klabu hiyo, kwani hawezi kuwasiliana na wachezaji wenzake wala hakai nao pamoja kantini na bado anaonesha wazi nia yake ya kutaka kuondoka.

Ronaldo amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba baada ya kurejea klabuni hapo kutoka Juventus msimu uliyopita, lakini anataka United wamuacha aondoke majira haya ya joto.

Sasa suala hili kocha Ten Hag, mtendaji mkuu Richard Arnold na mkurugenzi wa soka John Murtough waweripotiwa kulifanyia kazi kabla ya dirisha la usajili kufungwa tarehe 1 Septemba. United wako mkiani mwa ligi kuu ya England na watacheza dhidi ya Liverpool Jumatatu ijayo Agosti 22.