Jumatatu , 24th Jan , 2022

Timu ya Taifa ya Tanzania ya wanawake chini ya miaka 20 ''Tanzanite'' imeondoka Zanzibar kuelekea Karatu mkoani Arusha kwa kambi ya maandalizi ya mchezo wa marudiano wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya timu ya taifa ya Ethiopia utakaochezwa mapema mwezi ujao.

Wachezaji wa Tanzanite wakishangilia goli dhidi ya Ethiopia

Tanzanite imeondoka visiwani Zanzibara leo baada ya hapo jana kushinda bao 1-0 dhidi ya Ethiopia kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza ambao umechezwa katika uwanja wa Amaan  Zanzibar. Bao pekee la mchezo huo limefungwa na Christer John dakika ya 64 kwa mpira wa adhabu (free kick).

Kwa mujibu wa katibu mkuu wa shirikisho la soka nchini TFF Wilfred Kidao aliweka wazi kuwa kikosi hicho kitaweka kambi Karatu kwa sababu hali ya hewa ya huko inafanana na ile ya Ethiopia ambapo Tanzanite itacheza mchezo wa mkondo wa pili dhidi ya wenyeji wao Ethiopia utakaochezwa kati ya Februari 4 mpaka 6 2022.

Mshindi wa jumla wa mchezo wa Tanzania na Ethiopia atacheza na mshindi wa jumla wa mchezo kati ya Ghana na Uganda kwenye hatua inayofata na tayari mchezo wa mkondo wa kwanza Ghana inaongoza 2-1. Afrika itawakilishwa na timu mbili tu kwenye fainali za kombe la Dunia za wanawake chini ya umri wa miaka 20 zitakazofanyika nchini Costa Rica mwezi Agosti mwaka huu.