Ijumaa , 12th Jan , 2018

Pamoja na Tanzania kutolewa na Rwanda kwenye michuano ya kuwania kufuzu fainali za AFCON 2018 kwa wachezaji wa ndani (CHAN), lakini Rais wa TFF ameteuliwa kufungua michuano hiyo.

Shirikisho la Soka Barani Afrika CAF limemteua Rais wa shirikisho la soka nchini TFF Wallace Karia kuwa kamishna wa mechi ya ufunguzi wa fainali za ndani (CHAN) kati ya wenyeji Morocco dhidi ya Mauritania itakayochezwa kesho Januari 13.

Michuano hiyo ambayo inafanyika kwa mara ya tano tangu ianzishwe, inatarajiwa kuanza kesho ikishirikisha nchi 16 na itamalizika Februari 4, 2018 nchini Morocco.

Kabla ya Morocco kupewa uenyeji wa michuano hiyo awali ilikuwa ifanyike nchini Kenya ambapo shirikisho la soka Afrika CAF lilibadilisha kutokana na Kenya kushindwa kumaliza maandalizi ndani ya wakati.

Tanzania iliondolewa na Rwanda kwenye hatua ya kuwania kufuzu baada ya kutoka sare kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa CCM Kirumba kabla ya kushinda mchezo wa pili uliopigwa nchini Rwanda.