Jumatano , 14th Jul , 2021

Miongoni mwa stori 6 kali za 'Sports Countdown' za East Africa redio inamhusu mwanadada, Johanna Konta raia wa England kujitoa kutoshiriki mashindano ya Tennis kwenye Olympic inayotaraji kuanza Julai 24, 2021 nchini Japan baada ya kukutwa na Covid-19.

Johanna Konta wa England aliyepata Covid-19 na kujitoa kushiriki Oympic nchini Japan.

6 - Ni idadi ya mabao yaliyofungwa na wachezaji wawili wa klabu ya Werder Bremen ya nchini Ujerumani, kiungo Leonardo Bitterncourt na Joshua Sargent wakati timu yao ilipoishushia kipigo kizito kichwani  klabu ya Oberneuland cha mabao 12-0 kwenye wa mchezo wa kirafiki uliochezwa usiku wa kuamkia leo nchini Ujerumani.

Mabao mengine ya Bremen yamefungwa na Niclas Fulkurg na Kebba Badjie waliofunga mawili kila mmoja huku Romano Schmid na Ilia Gruev waliofunga bao moja moja.

Kwa upande mwingine, Washika mitutu wajiji la London klabu ya Arsenal wamepewa za uso baada ya kufungwa 2-1 na timu ya Hibernian ya nchini Scotland na kuanza vibaya kampeni  kabla ya msimu ujao huku kocha wake Mikel Arteta akisema hakuna kisingizio cha kujifichia kwenye kichapo hicho.

5 - Ni idadi ya mataji ya ligi kuu nchini aliyoyashinda kiungo mrwanda wa Yanga, Haruna Niyonzima ambapo klabu hiyo imewataka mashabiki wake kujitokeza kwa wingi siku ya Alhamisi Julai 15 mwaka huu Yanga itakapocheza dhidi ya IHEFU saa 10 kwenye dimba la mkapa jijini Dsm  kumuaga mchezaji huyo ambaye ataondoka mwishoni mwa msimu huu baada ya mkataba wake kumalizika na mabingwa hao wakihistoria nchini.

Niyonzima aliyejiunga na Yanga mwaka 2011 akitokea klabu ya APR ya nchini Rwanda anatajwa kuwa ni miongoni mwa wachezaji bora wakigeni kuwahi kuicheza nchini kufuatia kupata mafanikio makubwa ya kutwaa mataji na vilabu vya Yanga na Simba ikiwemo kushiriki kwenye historia ya Simba kucheza robo fainali ya klabu bingwa Afrika.

4 - Ni idadi ya mashtaka yanayolikabili shirikisho la soka nchini England 'FA' kutoka kwa shirikisho la soka barani Ulaya 'UEFA'  ambao wamefungua uchunguzi kuchunguza matukio yasiyoyakiungwana yaliyofanywa na mashabiki wa timu hiyo kwenye mchezo wa fainali ya UEFA EUROS iliyochezwa Julai 11 ambapo Italy iliifunga England kwa penalti 3-2 na kuwa mabingwa.

Mashtaka hayo ni, mashabiki wa England kuvamia uwanja wakati mchezo unaendelea, mashabiki kurushiana vifaa mbalimbali kwa lengo la kushambulia, mashabiki wa England kufanya usumbufu wakati timu ya taifa ya Italy inaimba wimbo wa taifa na mashabiki hao kutumia fataki uwanjani.

3 - Ni idadi ya timu zinazopatikana katika kila kundi la michuano ya timu za taifa za vijana chini ya umri wa miaka 23 kutoka ukanda wa Afrika mashariki na kati yaani 'CECAFA U-23 Challenge Cup' ambayo yamewekwa wazi hapo jana na Shirikisho la soka nchini TFF na kutaraji kuanza Julai 17 nchini Ethiopia.

Kundi A lina timu za vijana za Uganda, Tanzania nq DR Congo, kundi B lina wenyeweji Ethiopia, Burundi na Eritrea wakati kundi C lina Djibouti, Afrika Kusini na Kenya.

2 - Ni michezo ya kirafiki ya timu za taifa kwa upande wa mpira wa kikapu ambapo timu ya taifa ya Marekani ambao ni mabingwa wa kihistoria wa mashindano ya Olympic, wamepata ushindi wake wa kwanza wa alama 108 -80 dhidi ya timu ya Argentina baada ya kufungwa michezo yake miwili ya mwanzo dhidi ya Australi na Nigeria.

Australia wameifunga Nigeria kwa alama 108-69 kwenye muendelezo wa michezo ya kirafiki ambayo ni sehemu ya maandalizi kuelekea mashindano ya Olympic yatakayofanyika nchini Japana kuanzia Julai 24.

Na kwa upande mwingine, timu ya Phoenix Suns itacheza ugenini dhidi ya Milwaukee Bucks alfajiri ya kuamkia kesho kwenye mchezo wa nne wa fainali ya ligi ya kikapu nchini Marekani ambao Suns wanaongoza series 2-1.

1 - Ni nafasi ya ubora anayoshikilia mwanadada, Johanna Konta kwenye viwango vya tennis nchini England ambapo usiku wa kuamkia leo imethibitishwa kuwa amejitoa kushiriki michuano ya Olympic itakayofanyika nchini Japan na hii baada ya moja nyota huyo kukutwa na maambukizi ya Covid-19 aliyoambukizwa na moja ya wasaidizi wake kutoka kwenye kambi yake kuripotiwa kupata ugonjwa huo wiki moja iliyopita.

Hii ni mara ya pili Konta kukosa michuano mikubwa ya tennis mwaka huu ikumbukwe alishindwa kushiriki michuano ya tennis ya wimbledon baada ya covid-19 kutinga kwenye kambi yake.