Alhamisi , 15th Jul , 2021

Ligi kuu soka Tanzania bara itaendelea leo Julai 15, 2021 kwa michezo yote tisa ambapo mchezo utakaowakutanisha vigogo ni ule wa mabingwa wa ligi, Simba itakapocheza dhidi ya Azam saa 1:00 usiku kwenye dimba la Chamazi jijini Dar es Salaam.

Winga wa Simba, Jose Luis Miquissone akifanya jaribio la kufunga bao mbele ya mlinda mlango wa Azam, Mathias Kigonya kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza wa VPL ambao uliisha kwa sare ya mabao 2-2.

Mchezo huo utaambatana  na matukio moja kubwa la klabu ya Azam kukiri kupitia Mkurugenzi wake wa Habari na Mawasiliano, Zakaria Thabit 'Zakazakazi' kuwa watawapigia makofi ya heshima 'Guard of Honour' mabingwa hao pindi waingiapo uwanjani kabla ya mchezo kuanza.

Zakaria amesema, “Sisi Azam Sports Club tutafanya 'Guard of Honour' kwa simba, kama mabingwa tutawapa heshima hiyo, tutapiga makofi ya heshima”.

Azam ndiyo ilikuwa klabu pekee kufanyiwa 'Guard of Honour' walipokuwa mabingwa msimu wa mwaka 2013-2014 dhidi ya  JKT Ruvu April 19, 2014 na kuandika historia hiyo ya kujivunia nchini.

Kuelekea kwenye mchezo huo, kocha msaidizi wa wenyeji Azam, Mrundi Bahati Vivier amethibitisha kuwakosa mlinzi wake wakati na nahodha, Aggrey Morris, kiungo Salum Aboubakar 'Sure boy' na mshambuliaji wake tegemeo, Prince Dube ambao wote wanasumbuliwa na majeraha.

Kwa upande wa Simba, Selemani Matola ambaye ni kocha msaidizi wa mabingwa hao ameweka wazi kuwa, Jonas Mkude atakosekana kutokana na kuendelea kusimamishwa kufuatia sakata lake la utovu wa nidhamu tokea mwezi uliopita.

Bernard Morris yupo nchini kwao Ghana kutokana na sababu za kifamilia licha ya kwamba anataraji kurejea nchini hii leo, Ibrahim Ajib anasumbuliwa na Malaria ilhali Miraji Athumani ana majeraha.

Simba ipo nafasi ya kwanza ikiwa na alama 79 wakati Azam ipo nafasi ya tatu ikiwa na alama 64 baada ya wote kucheza michezo 32.

Mchezo mwingine ni ule wa Yanga dhidi ya Ihefu utakaochezwa saa 10:00 jioni kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ukiambatana na tukio la kumuaga kwa heshima kiungo wake mchezeshaji, Haruna Niyonzima.

Michezo mingine itakayopigwa saa 8:00 mchana ni KMC dhidi ya JKT Tanzania, Ruvu Shooting itakipiga na Namungo wakati Tanzania Prisons watacheza dhidi ya Biashara United Mara.

Michezo itakayochezwa saa 10:00 jioni ipo minne, ambapo Coastal Union itacheza dhidi ya Mwadui, Dodoma Jiji na Mtibwa Sukari, Mbeya City na Gwambina ilhali Polisi Tanzania atakipiga na Kagera Sukari.