Salah amlilia Mane

Friday , 13th Oct , 2017

Winga wa Liverpool Mohamed Salah amesema kuwa majeruhi ya mchezaji mwenzake Sadio Mane ni habari mbaya kwa timu nzima.

Salah amesema hayo baada ya kurejea nchini Uingereza kwaajili ya maandalizi ya mchezo wa ligi kuu ya soka nchini England kati ya timu yake ya Liverpool dhidi ya Manchester United kesho.

“Ni kweli hatutakuwa na Mane kwenye mchezo dhidi ya Manchester United lakini tunatakiwa kuungana na kucheza kama timu, habari za majeruhi ya Sadio Mane zilikuwa mbaya sana kwa kila mmoja ndani ya timu”, amesema Salah.

Salah aliiongoza Misri kufuzu fainali za kombe la Dunia 2018 nchini Urusi kwa mara ya kwanza tangu ifanye hivyo mwaka 1990, wakati Mane aliumia akiwa kwenye majukumu ya timu yake ya taifa ya Senegal.

Mchezo huo utapigwa kesho saa 14:30 kwa saa za Afrika Mashariki ambapo Manchester United itaendelea kumkosa Paul Pogba pamoja na Marouane Fellaini wakati Liverpool itamkosa Sadio Mane. Manchester United ipo nafasi ya 2 ikiwa na alama 19 wakati Liverpool ipo katika nafasi ya 7 ikiwa na alama 12.