Alhamisi , 15th Sep , 2022

Baada ya sekeseke la kuzuiwa kucheza kwa winga mpya wa Yanga, Tuisila Kisinda na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) sasa ni rasmi nyota huyo atacheza

Kisinda aliyerejea Yanga kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea RS Berkane ya Morocco hapo awali alizuiliwa kucheza kwa kile kilichodaiwa Yanga ilitimiza idadi ya wachezaji wa kigeni (12) kabla ya ujio wa Mkongomani huyo.

Leo TFF imetoa taarifa rasmi ya kumruhusu Kisinda kuichezea Yanga baada ya timu hiyo kumuondoa mshambuliaji Mzambia Lazarous Kambole kwenye usajili wa awali.

Katika taarifa hiyo, TFF imehalalisha kucheza kwa Kisinda kuichezea Yanga ikiwa ni uamuzi wa kamati ya Sheria na hadhi za wachezaji ya TFF.

Hilo limetimia baada ya kumpeleka kwa mkopo Kambole katika timu ya Wakiso Giants nchini Ugands na tayari ITC yake imetumwa huko na sio Yanga tena.

Yanga mechi ijayo itacheza dhidi ya Ihefu mkoani Mbeya na Kisinda anaweza kuwa sehemu ya mechi hiyo.