Alhamisi , 10th Nov , 2022

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameipongeza Yanga SC kwa kuifunga Club Africain ya Tunisia na kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Yanga ilitinga katika hatua hiyo Jumatano Novemba 9 mwaka huu baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Club Africain.

Ujumbe wa salamu za pongezi kwa Yanga ulioandikwa leo kwenye ukurasa rasmi wa Rais Samia katika mtandao wa Instagram unasomeka;

"Kongole Yanga SC kwa kwa ushindi na kufanikiwa kusonga mbele katika michuano ya soka la wanaume kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, msimu wa 2022/2023. Nawatakia kila la heri katika hatua inayofuata,"

Yanga inatinga hatua ya makundi kwenye kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuondolewa Ligi ya mabingwa Afrika na miamba ya soka ya Sudan, Al Hilal.

Mechi ya kwanza Yanga ikiwa nyumbani dhidi ya Club Africain ilitoka suluhu katika Uwanja Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na kwenda kupata matokeo ya ushindi Tunisia.

Mara ya mwisho kwa Yanga kwenda hatua ya makundi ya mashindano hayo ilikuwa mwaka 2018 huku shauku na imani ya mashabiki wa soka nchini ikiwa ni kuiona ikifika mbali katika mashindano hayo.