Ijumaa , 2nd Dec , 2022

Aliyewahi kuwa kocha wa zamani wa Yanga, Mwinyi Zahera raia wa Congo DR amejiunga na klabu ya Polisi Tanzania ya mkoani Kilimanjaro kuwa kocha mkuu baada ya kufikia makubaliano na uongozi wa timu hiyo.

Zahera ambaye alikuwa mkurugenzi wa kukuza soka la vijana Yanga, amejiunga na timu hiyo leo akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Joslin Bipfubusa raia wa Burundi ambaye mkataba wake ulisitishwa Oktoba 26, 2022 kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo, miezi mitatu tangu ajiunge nayo Julai 26.

Ikiwa chini ya Mrundi huyo, Polisi Tanzania ilicheza mechi tisa ikiambulia pointi tano tu baada ya kushinda moja, sare mbili na kufungwa sita, ambapo alitimuliwa baada ya kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Tanzania Prisons.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma ya klabu hiyo ambayo imechapishwa kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, makubaliano hayo yamefikiwa leo Desemba 2, 2022 mkoani Kilimanjaro baada ya mazungumzo ya muda mrefu na tahmini ya kina ya kuhitaji kufanya vizuri.

Taarifa hiyo ambayo imetolewa Afisa habari wa klabu hiyo, Frank Lukwaro imewaomba mashabiki na wadau kumpa ushirikiano kocha huyo katika kuliongoza benchi la ufundi.

"Klabu ya Polisi Tanzania inapenda kuujulisha umma na mashabiki wake  kuwa imefikia makubaliano na ndugu Mwinyi Zahera kuwa kocha Mkuu wa timu yetu,"

"Makubaliano na kocha Zahera yamefikiwa leo (Ijumaa) mkoani Kilimanjaro baada ya mazungumzo ya muda mrefu pamoja na tathmini ya kina kwa lengo la kufanya vizuri. Tunawaomba mashabiki na wadau wote kumpa ushirikiano Kocha Zahera katika majukumu yake," imesema taarifa hiyo.

Baada ya kuondolewa Bipfubusa, Polisi Tanzania ilikuwa chini ya Kocha John Tamba ambaye ameiongoza katika michezo mitano ya Ligi Kuu akishinda mmoja dhisi ya Ihefu, sare na Dodoma Jiji na kupoteza dhidi ya Singida Big Stars, Mtibwa Sugar na Simba.