Alhamisi , 23rd Jun , 2022

Beki wa kimataifa wa Kenya, Joash Onyango ameongeza mkataba wa miaka miwili kuendelea kusalia katika klabu hiyo ya Simba SC baada mkataba wake wa awali kumalizika mwisho wa msimu huu.

Beki wa kimataifa wa Kenya, Joash Onyango .

Akizungumza na EATV Onyango amesema kuwa amesaini mkabata wa miaka mwili ambapo ataendelea kuwatumia Simba hadi mwaka 2024.

''Wanasimba watulie kwakuwa sasa tumepoteza ubingwa lakini msimu ujao tumejipanga kufanya vyema katika michuano yote ambayo tutashiriki na kurudisha heshima ilikuwa nayo Simba'' amesema Onyango.

Tangu alipojiunga na Simba, Onyango amecheza sehemu muhimu ya timu akiwa kama beki wa kati ambapo amekuwa akisaidiana na beki kisiki kutoka Congo, Eneck Inonga, Kennedy Juma pamoja na Pascal Wawa ambaye kwasasa hatokuwepo kwenye kikosi cha Wanamsimbazi msimu ujao.

Hata hivyo kulikuwa na hofu juu ya mustakabali wa Onyango baada ya kukosa mechi mbili za mwisho za Simba dhidi ya Mbeya City na KMC huku Mei mwaka jana, vigogo wa Afrika Kusini, Orlando Pirates, walionyesha nia ya kutaka kuwasajili wachezaji hao na aliyekuwa Msemaji wa Simba wakati huo, Haji Manara (sasa Yanga SC) akadai kitita cha Sh100 milioni.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 anakuwa mchezaji wa pili ndani ya klabu ya Simba kuongezewa mkataba ambao wa kwanza ni Aishi Manula ambaye aliongezewa mkataba siku chache zilizopita huku Rally Bwalya, Bernard Morrison na Pascal Wawa wakiondoka klabu hapo.