Jumatatu , 18th Jun , 2018

Nyota wa Brazil Neymar Jr, jana alijiwekea rekodi ya pekee japo haikuwa na msaada kwa timu yake, baada ya kuchezewa faulo mara nyingi zaidi kuliko mchezaji yoyote tangu alipofanyiwa hivyo Alan Shearer wa England mwaka 1998.

Katika mchezo huo wa kwanza kwa Brazil kwenye fainali za mwaka huu dhidi ya Switzerland, Neymar alichezewa jumla ya faulo 10, ikiwa ni mara nyingi zaidi tangu alipofanyiwa hivyo Alan Shearer mara 11 kwenye mchezo kati ya England na Tunisia.

Neymar Jr alitegemewa kuibeba nchi yake kwenye mchezo huo,lakini haikuwa hivyo baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Switzerland. Bao  la Brazil lilifungwa na kiungo Philippe Coutinho huku lile la Switzerland likifungwa na Steven Zuber.

Brazil jana ilishindwa kupata ushindi kwenye mchezo wake wa ufunguzi kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1934 ilipofungwa mabao 3-1 na Hispania. Katika mechi zake 21 za Kombe la Dunia Brazil imeshinda 16, sare 3 na kufungwa mara 2.

Brazil sasa inashika nafasi ya 2 kwenye Kundi E ikiwa nyuma ya Serbia ambayo ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Costa Rica huku Switzerland ikishika nafasi ya 3 na Costa Rica ikishika mkia.