Jumanne , 15th Oct , 2019

Jana imeshuhudiwa sare nyingine ya kikosi cha Taifa Stars katika mechi za hivi karibuni, baada ya kutoka suluhu ya bila kufungana na wenyeji Rwanda katika mchezo wa kirafiki.

Kocha Etienne Ndayiragije

Mpaka sasa Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije ameiongoza Stars katika mechi 5, akiwa hajashinda mechi yoyote ndani ya dakika 90 za mchezo. Mchezo wa kwanza dhidi ya Kenya uliofanyika katika uwanja wa taifa, Taifa Stars ilitoka sare ya bila kufungana na mchezo wa pili ilishinda kwa mikwaju ya penalti nchini Kenya na kufuzu makundi kuwania kufuzu Kombe la Dunia.

Mchezo wa tatu uliofuata, Etienne Ndayiragije aliiongoza Stars kwa kucheza dhidi ya Burundi kuwania kufuzu michuano ya CHAN na mchezo huo uliisha kwa sare ya bao 1-1, ambapo Stars ikaibuka mshindi katika mikwaju ya penalti iliyowapeleka kukutana na Sudan katika hatua nyingine.

Kwenye mchezo dhidi ya Sudan katika uwanja wa taifa, Stars ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 ambapo hivi sasa ina kibarua cha kushinda ugenini ili iendelee katika hatua inayofuata kufuzu CHAN.

Baadhi ya mashabiki wameanza kuonesha mashaka juu ya matokeo ya Taifa Stars chini ya Ndayiragije, wakitaka hatua zichukuliwe haraka za kumpata kocha mkuu, lakini wengine wakipendekeza kocha huyo kupewa muda zaidi kwakuwa ni kocha anayeufahamu vizuri mpira wa Tanzania na wachezaji wake.

Shinikizo linaweza kuwa kubwa zaidi katika mchezo wa marudiano dhidi ya Sudan unaofuata hivi karibuni. Jambo ambalo Ndayiragije anatakiwa kulifikiria zaidi ni kufanya kila aina ya mbinu ili Stars ipate matokeo mazuri na kusonga mbele ili kuondoa maswali yaliyoanza kuibuka kwa Watanzania wapenda soka.