Jumamosi , 25th Nov , 2017

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Dk. Harrison Mwakyembe kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi  katika mchezo wa uzinduzi wa Ligi Kuu soka ya Wanawake Tanzania Bara.

Ligi hiyo inaanza kesho Novemba 26, 2017 kwenye vituo viwili vya Dar Es Salaam na Arusha ambapo kundi A litakuwa Dar es Salaam likitumia Uwanja wa Karume wakati kundi B litakuwa Arusha likitumia Uwanja wa General Tyre. Mchezo wa ufunguzi utakuwa kati ya Panama FC itakayocheza na Alliance Queens.

Mbali ya Dk. Mwakyembe, wageni wengine wanaotarajiwa kuwepo kwenye uzinduzi huo ni mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, Rais wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia na kaimu katibu mkuu wa TFF, Kidao Wilfred pamoja na viongozi wengine.

Kundi A lina timu za Mlandizi Queens ya Pwani, JKT Queens ya Dar es Salaam, Fair Play ya Tanga, Simba Queens ya Dar es Salaam, Ever Green Queens ya Dar es Salaam na Mburahati Queens ya Dar Es Salaam.

Kundi B lenyewe linajumuisha timu za Marsh FC ya Mwanza, Kigoma Sisters ya Kigoma, Panama FC ya Iringa, Baobab Queens ya Dodoma, Alliance Queens ya Mwanza na Majengo Queens ya Singida.