Msuva aendelea kutisha Morocco

Thursday , 12th Oct , 2017

Winga wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva jana ameifungia timu yake, Difaa Hassan El - Jadida bao muhimu la ugenini ikifungwa 2-1 katika mchezo wa Kombe la Ligi Morocco na Chabab Rif Hoceima Uwanja wa Mimoun Al Arsi mjini Al Hoceima.

Kwa bao hilo, Difaa Hassan El – Jadida watahitaji ushindi wa 1-0 tu nyumbani kwenye mchezo wa marudiano wiki ijayo ili kusonga mbele kwenye michuano hiyo. 

“Nina furaha nimefunga bao, japokuwa tumefungwa 2-1 lakini kwenye mchezo wa ugenini, tunaelekeza nguvu zetu kwenye mchezo wa marudiano tuweze kushinda na kusonga mbele,”amesema Msuva akizungumza mapema leo"  alisema Msuva

Huo ni mwendelezo wa mwanzo mzuri kwa Msuva tangu ahamie timu hiyo miezi miwili iliyopita kufuatia kucheza Tanzania kwa muda mrefu.

Na hilo linakuwa bao lake la nane tangu amejiunga na timu hiyo la pili kwenye mechi za mashindano, mengine sita akifunga kwenye mechi za kirafiki, zikiwemo za ziara ya Hispania.  

Msuva alisaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na DHJ Julai 28, mwaka huu baada ya kucheza Yanga ya nyumbani, Tanzania tangu mwaka 2012 akitokea Moro United iliyokuwa tayari imehamishia maskani yake Dar es Salaam kutoka Morogoro.